Homa ya mapafu ni aina ya
maambukizi yanayoathiri mapafu. Ni ugonjwa ambao unaua watoto wengi hasa katika
nchi zinazoendelea duniani. Inakadiriwa kwamba watoto karibu milioni 1.6 walio
chini ya miaka 5 wanakufa kila mwaka kutokana na ugonjwa huu. Kutokana na vifo
vingi vinavyotokana na homa ya mapafu tarehe 12 ya mwezi wa Novemba kila mwaka
imefanywa kuwa siku rasmi ya homa ya mapafu duniani, ambapo nembo ya siku hiyo
ni nguo za rangi ya bluu.
Muundo wa Mapafu
Mapafu yanajumuisha mirija
mikubwa ya hewa (bronchi) ambayo hugawanyika kufanya mirija midogo zaidi
ya hewa (bronchioles), ambayo nayo hutengeneza vifuko vidogo vidogo ya
hewa (alveoli). Vifuko hivi vidogo vya hewa (alveoli) vina
mishipa ya kupitisha damu (capillaries) ambayo husaidia kuchuja na
kusafirisha hewa safi ya oksijeni tunayovuta kuingia kwenye damu na hewa chafu
ya ukaa (kaboni dioksidi) kuondolewa kwenye damu na kuingizwa kwenye mapafu
tayari kwa kutolewa nje ya mwili.
Kwa kawaida vifuko hivi vidogo
hujaa hewa muda wote tayari kwa kusafirishwa. Inapotokea mtu akapata homa ya
mapafu, vifuko hivi hujaa maji au usaha hivyo kuathiri upitishaji wa hewa safi
kwenye damu na kusababisha tatizo la kupumua.
Homa ya mapafu husababishwa na nini?
Kuna aina kadhaa ya vimelea ambao
vinaweza kusababisha maambukizi ya mapafu. Vimelea hivi hujumuisha bakteria,
virusi, parasite na fangasi.Vimelea hawa hushambulia mwili wa binadamu
kulingana na umri na kinga ya mwili. Kwa mfano, bakteria wanaosababisha homa ya
mapafu kwa watoto wachanga ni tofauti na wale wanaosababisha ugonjwa huo kwa
watoto wakubwa.
Baadhi ya vimelea wa bakteria
wanaoshambulia watoto ni pamoja na Streptococcus pneumoniae ambao
ni aina ya bakteria wanaoongoza kusababisha homa ya mapafu kwa watoto. Wapo pia Haemophilus
influenzae aina b (Hib) ambao ni aina ya pili ya bacteria walio
maarufu zaidi kwa kusababisha ugonjwa wa homa mapafu kwa watoto. Staphylococcus
aureus ni aina nyingine ya bacteria ambao hushambulia zaidi watoto
wachanga. Kuna pia Group B streptococci ambao pia hushambulia
zaidi watoto wachanga.
Kwa upande wa virusi, virusi wa
aina ya Respiratory syncytial virus ndiyo wanaoongoza kwa
kusababisha homa ya mapafu kwa watoto.
Aidha, vimelea wa Pneumocystis
jiroveci ambao kwa sasa huwekwa kwenye kundi la parasite ni maarufu
zaidi miongoni mwa parasite wanaosababisha homa ya mapafu kwa watoto wenye
upungufu wa kinga mwilini hususani watoto wenye VVU.
Aina nyingine za bakteria ambao
hushambulia zaidi watoto wakubwa ni pamoja na Mycoplasma pneumonia naChlamydia
pneumonia.
Jinsi Homa ya Mapafu inavyoenezwa
Kuna namna nyingi za kuenea kwa
homa ya mapafu. Kwa kawaida, virusi na bacteria hupatikana katika sehemu ya juu
ya mfumo wa njia ya upumuaji (upper respiratory tract). Inapotokea kinga
ya mwili ya mtoto imeshuka kwa sababu yeyote ile, vimelea hivi huweza kusambaa
na kufika mpaka sehemu ya chini ya mfumo wa njia ya upumuaji (lower
respiratory tract) na hatimaye kushambulia mapafu. Hali kadhalika, vimelea
hawa wanaweza kuenea kwa njia ya damu kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kabla ya
kuzaliwa yaani kipindi cha mimba.
Dalili za ugonjwa wa homa ya mapafu
Dalili za vichomi au homa ya
mapafu kwa watoto hutegemea na umri wa mtoto. Kwa watoto wadogo, dalili za
awali zinaweza kuwa homa kali pamoja na mtoto kuhangaika na kunyong’onyea.
Watoto wanaozaliwa wakiwa na uambukizi wa bacteria aina ya Streptococcus kundi
B wanaweza kuwa na homa na kupumua kwa shida. Wakati mwingine mtoto anaweza
kuwa na dalili ambazo si maalum (no-specific symptoms) kama vile
kuhangaika na kushindwa kunyonya au kula vizuri bila kuwa na dalili yeyote ya
kushindwa kupumua. Hali hii inaweza kutokea kwa mtoto wa umri wowote ule.
Dalili za kawaida za homa ya mapafu ambazo huwapata karibu watoto wote
wanaoathirika na ugonjwa huu ni pamoja na:
homa
Kuhisi baridi
kikohozi
Kupumua kwa haraka kuliko kawaida
kutoa sauti isiyo ya kawaida
wakati wa kupumua
Mbavu za mtoto kuingia ndani
wakati wa kupumua
maumivu ya tumbo
kupoteza hamu ya kucheza
kupoteza hamu ya kula na
kushindwa kunyonya
Mtoto kubadilika rangi na kuwa na
rangi bluu katika midomo na kucha
Hata hivyo, si lazima dalili zote
hizi ziwepo kwa kila mtoto. Baadhi ya watoto huonesha kupumua kwa haraka kama
dalili pekee ya homa ya mapafu. Iwapo vimelea vimeshambulia sehemu za chini ya
mapafu karibu ya tumbo, sehemu ijulikanayo kama kiwambo au diaphragm,
mtoto anaweza asioneshe hali yeyote ya kushindwa kupumua ingawa anaweza kuwa na
homa na kujihisi maumivu makali ya tumbo, vichomi na pia kutapika.
Watoto wachanga wanaweza
kushindwa kunyonya, na pia kupoteza fahamu na kupata degedege.
Vihatarishi vya homa ya mapafu (risk
factors)
Katika hali ya kawaida kinga ya
mtoto mwenye afya njema humlinda asishambuliwe na vimelea vinavyosababisha
magonjwa mbalimbali. Hali huwa ni tofauti pale ambapo kinga ya mtoto ni ndogo
au dhaifu, kwa vile mfumo mzima wa ulinzi huathirika na hivyo basi inakuwa ni
rahisi kwa mtoto kupata homa ya mapafu.
Mfumo wa kinga wa mtoto unaweza
kuwa dhaifu kwa ukosefu wa lishe bora hasa kwa watoto wachanga ambao
hawanyonyeshwi ipasavyo. Aidha uwepo wa magonjwa mengine, kwa mfano, maambukizi
ya VVU, saratani na ugonjwa wa Surua hupelekea kinga ya mwili kuwa dhaifu.
Lakini vile vile kuna mazingira
yanayoweza kusababisha mtoto kuwa katika hatari ya kupata homa ya mapafu mfano
moshi wa sigara, au moshi ndani ya nyumba unaosababishwa na kupikia kuni au
mkaa. Vilevile msongamano ndani ya nyumba kutokana na watu kuwa wengi sehemu
moja nayo huweza kusababisha watoto kupata homa ya mapafu.
Uchunguzi na Vipimo
Daktari humchunguza mtoto mgonjwa
kwa kusikiliza dalili za ugonjwa kutoka kwa mzazi/mlezi wa mtoto, kuchunguza
viashiria vya ugonjwa huu na kisha kumpima mtoto kwa kutumia kifaa
kinachosaidia kusikia sauti mbalimbali katika mfumo wa hewa wa mgonjwa
kiitwacho stethoscope.
Ili kujiridhisha na kuwa na uhakika wa tatizo
hili, vipimo vifuatavyo vinaweza kufanywa kulingana na mazingira na upatikanaji
wake. Vipimo hivyo ni pamoja na X-ray ya kifua, au CT-scan ya kifua, pamoja na
damu ili kuchunguza madhara yaliyoletwa na homa hii ya mapafu.
Faida ya kipimo cha CT-scan ni
ule uwezo wake wa kutofautisha aina tofauti za homa ya mapafu na aina
ijulikanayo kama Atypical pneumonia ambayo si rahisi kuonekana
kwa kutumia X-ray ya kawaida ya kifua. X-ray ya kifua na CT-scan ya kifua kwa
pamoja vina uwezo wa kuonesha tatizo hata pale ambapo daktari ameshindwa
kusikia sauti maalum kwa kutumia kifaa chake cha stethoscope.
Matibabu
Maamuzi ya Matibabu kwa watoto
wenye homa ya mapafu hutegemea aina ya vimelea, umri na hali ya mtoto. Mara
nyingi antibiotics ndizo hutumika katika kutibu homa ya mapafu inayosababishwa
na maambukizi ya bakteria. Kwa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi,
antibiotics hazina uwezo wowote wa kutibu. Ieleweke kuwa ni tabibu anayeweza
kufahamu kama mtoto wako anahitaji antibiotics au dawa za aina nyingine,
kwahiyo ni muhimu kwa mzazi ama mlezi kumpeleka mtoto hospitalini haraka pindi
mtoto anapoonesha dalili za ugonjwa huu badala ya kuamua kumpa dawa bila
kufuata ushauri wa wataalamu wa afya.
Kama
una swali,maoni au ushauri wasiliana nasi kwa simu namba
0769368546,0754301115,0764 293333,0672 666601,0719097574 na 0685 220190 pia
www.facebook.com/lupimoclinic,www.twitter.com/lupimoclinic na
www.hulkshare.com/lupimoclinic.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni