Ijumaa, 26 Februari 2016

KULA NYANYA UJIEPUSHE NA KIHARUSI

SOTE tunajua ugonjwa wa kiharusi (stroke) ni miongoni mwa magonjwa hatari kwani ukikupata unaweza kudhoofisha baadhi ya viungo vyako vya mwili kama siyo vyote na kukufanya ushindwe kufanya kazi zako za kawaida na kuwa mtu wa ndani tu kwa maisha yako yote.

Lakini unaweza kujiepusha na ugonjwa huo hatari kwa kuzingatia ulaji wa vyakula sahihi pamoja na kufanya mazoezi. Utafiti wa hivi karibuni umebaini kwamba nyanya (tomatoes) hutoa kinga mwilini dhidi ya ugonjwa wa kiharusi au kupooza kama unavyojulikana na wengine.
 

Hivi karibuni, watafiti wa nchini Finland walifanya utafiti wa kina na kutoa taarifa kuhusu kirutubisho aina ya ‘lycopene’ kinachopatikana kwa wingi kwenye nyanya, matikitimaji na pilipili. Wamesema katika taarifa yao kuwa watu zaidi ya 1,000 waliowafanyia utafiti wenye kiwango kingi cha ‘lycopene’ kwenye mfumo wa damu zao, hawakuonesha dalili kabisa za kupatwa na kiharusi.
 

Aidha, Chama cha Taifa cha wenye Kiharusi cha nchini Marekani (The National Stroke Association) kimesema kuwa wanawake wengi hufariki dunia nchini humo kutokana na kiharusi kwa idadi sawa na wale wanaofariki kutokana na ugonjwa wa saratani ya matiti. Hii ina maana kwamba ugonjwa wa kiharusi nao ni tishio kama ilivyo kwa ugonjwa wa saratani ya matiti.
 

Utafiti mwingine katika eneo hilo umeonesha pia kuwa wanaume wana hatari kubwa zaidi ya kufariki dunia au kupatwa na matatizo mengi kutokana na ugonjwa wa kiharusi kuliko wanawake. Hivyo kati ya wanaume na wanawake, wanaume zaidi ndiyo hupatwa na kiharusi au matatizo yatokanayo na ugonjwa huo kuliko wanawake.

Utafiti huu mpya umeendelea kuthibitisha ukweli wa siku zote kuwa matunda na mbogamboga hutoa kinga katika mwili wa binadamu dhidi ya magonjwa mengi hatari, hivyo wito umetolewa tena wa watu kupenda kula matunda na mbogamboga hasa nyanya, matikitimaji pamoja na pilipili ambavyo vimeonekana kuwa na kinga kubwa zaidi mwilini.
 

Hata hivyo, imeelezwa kuwa baada ya matokeo ya utafiti huu, watu wamekumbushwa umuhimu wa kuendelea kula na aina nyingine ya matunda, kwani kila tunda au mboga ya majani ina faida na umuhimu wake katika mwili wa binadamu.
 

Mwisho imeelezwa kuwa ulaji wa nyanya za aina zote una faida, iwe ni ile inayopikwa pamoja na mboga au ile inayoliwa ikiwa imeiva bila kupikwa. Ni vizuri kuchangamkia ulaji wa vitu kama hivi ili kuipa miili yetu uwezo wa kujikinga wenyewe dhidi ya maradhi hatari, yakiwemo yale ya saratani ambayo kwa kiasi kikubwa huweza kuzuiwa kwa kula mboga za majani na matunda ya aina mbalimbali.

kwa maelezo zaidi,maoni au ushauri wasiliana nasi kwa simu namba 0769368546,0719097574 na 0742120577 pia www.facebook.com/lupimoclinic,www.twitter.com/lupimoclinic na www.hulkshare.com/lupimoclinictanzania.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni