ATHARI ZA MAGONJWA YA ZINAA KWA WAJAWAZITO
Magonjwa
ya zinaa ni maambukizi yaenezwayo kutoka mtu mmoja hadi mwingine kwa
kufanya ngono na mtu mwenye vimelea vya ugonjwa. Aina ya vimelea
vinavyohusika kusababisha magonjwa haya ni kama bakteria, virusi na aina
nyinginezo za vimelea vya magonjwa.
Kuna aina nyingi za magonjwa ya zinaa yanayojulikana, lakini baadhi ya
hayo ni kama kisonono, malengelenge, HIV/AIDS,Pangusa,Chlamydia, HPV(Human
Papilloma Virus),Kaswende, Trichomuniasis na mengineyo mengi.
Wanawake walio wajawazito waweza kuambukizwa magonjwa ya zinaa sawa na
wanawake wasio wajawazito. Magonjwa haya ya zinaa mengi huwa hayaonyeshi
dalili mtu anapoambukizwa, kwa hiyo ni vigumu wakati mwingine kwa kina
mama wenye mimba kugundua kama wameambukizwa magonjwa haya.Kina mama
walio wajawazito ni vyema kuhudhuria kliniki ili wafanyiwe uchunguzi wa
magonjwa ya zinaa ikiwepo HIV ambayo husababisha Udhaifu wa Kinga
Mwilini.Ni vyema kina mama wajawazito kufahamu madhara ya magonjwa haya
kwa afya zao pamoja na mimba inayokua tumboni. Wenza wa kina mama walio
athirika ni lazima nao waudhurie kliniki kwa ajili ya vipimo na
matibabu.
Magojwa ya zinaa yaweza kusababisha madhara makubwa kwa mama na mtoto. Baadhi ya madhara haya yaweza kuonekana wakati mtoto
anapozaliwa, lakini madhara mengine huendelea kujitokeza baada ya miezi
hata miaka mingi baadaye. Ugunduzi wa mapema ni muhimu kwa kuwa
maambukizi mengine ya magonjwa ya zinaa kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto
yaweza kuzuiliwa endapo itagundulika mapema, mfano yawezekana kuzuia
maambukizi ya HIV kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kwa kutumia dawa
maalum ambazo mama hupewa wakati wa ujauzito.
Kaswende ni ugonjwa ambao awali kabisa huambukizwa kwa kufanya
ngono,lakini waweza kuambukizwa kwa mtoto wakati wa ujauzito. Mtoto
anapoambukizwa ugonjwa huu hupelekea mtoto kupata matatizo ya kiafya.
Kaswende imekuwa ikihusika na kuzaliwa kwa watoto walio njiti, mtoto
kuzaliwa akiwa amekufa au hata pengine mtoto kufariki muda mfupi baada
ya kuzaliwa. Mtoto akiishi na asipotibiwa huweza kuathirika ogani za
mwili kama ubongo, macho, masikio, moyo, ngozi, meno na hata mifupa. Ni
vyema kila mama anayeudhuria kliniki kwa mara ya kwanza kuchunguzwa
endapo ana ugonjwa huu.
Kisonono ni ugonjwa ambao huambukizwa sana katika nchi za kusini mwa
jangwa la sahara.Ugonjwa huu usipotibiwa wakati wa ujauzito, waweza
kupelekea mimba kutoka,mtoto kuzaliwa akiwa njiti, uzito mdogo wakati wa
kuzaliwa, chupa ya uzazi kupasuka kabla ya wakati na uambukizi wa
majimaji yaliyomzunguka mtoto. Mtoto anaweza kuambukizwa ugonjwa huu
wakati wa kuzaliwa wakati anapotoka kupitia njia ya uzazi. Mtoto
asipotibiwa anaweza kupata uambukizi wa macho.
Trichomoniasis ni uambukizi katika uke wa mwanamama unasababishwa na kimelea kijulikanacho kama Trichomona vaginalis.Dalili
za ugonjwa hutofautina kutoka mwanamama mmoja hadi mwingine. Lakini
dalili zinapojitokeza huwa ni kuwashwa sana,harufu mbaya, kutoka
majimaji yenye harufu na kutoka damu baada ya tendo la ndoa. Kina mama
wenye dalili za ugonjwa ni vyema kuchunguzwa na kupatiwa matibu sahihi.
Uambukizi usiotibiwa unahusishwa na kujifungua kabla ya wakati,kupasuka
chupa ya uzazi kabla ya wakati na mtoto kuzaliwa akiwa na uzito mdogo.Ni
mara chache mtoto huambukiazwa ugonjwa wakati wa kuzaliwa.
Ugonjwa mwingine ni Hepatitis B ambao ni uambukizi katika ini usababishwao na virusi aina ya Hepatitis B
(HBV).Mama anaweza kumuambukiza mtoto wakati wa ujauzito, na hatari ya
uambukizi hutegemea ni wakati gani mama aliambukizwa ugonjwa. Hatari
huwa kubwa endapo mwanamama ataambukizwa ugonjwa anapokaribia
kujifungua.Mtoto mwenye ugonjwa kwa muda mrefu huwa katika hatari ya
kupata ugonjwa sugu wa ini au hata saratani ya ini baadaye katika maisha
yake.Uambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto waweza kuzuiwa kwa
upimaji wa mapema pamoja na kutoa tiba kwa mtoto mara baada ya kuzaliwa.
Hepatitis C ni uambukizi wa ini usababishwao na virusi vya Hepatitis C
(HCV), na huweza kuambukizwa kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa
ujauzito.Mara nyingi ugonjwa hupimwa kwa wale walio katika hatari ya
kuambukizwa ugonjwa huu, mfano wale wanaojidunga dawa za kulevya. Athari
za ugonjwa huu ni mama kujifungua kabla ya wakati na mtoto kuzaliwa
akiwa na uzito mdogo.Kwa kawaida watoto wanaoambukizwa huwa hawaonyeshi
dalili, na ugonjwa waweza kuisha wenyewe bila kutibiwa na hata kama
ugonjwa utajitokeza, huwa ni rahisi kuutibu kwa watoto ukilinganisha na
watu wazima.
Upimaji, pamoja na matibabu ya magonjwa ya zinaa ni muhimu kwa afya ya
mama mjamzito na mtoto atakayezaliwa. Kwa hiyo ni jukumu la wazazi
kujilinda na kujikinga na magonjwa haya kwa ajili ya afya yao na watoto
watakaozaliwa.
Ni vyema kwa kina mama wajawazito kuzungumza na daktari wao kuhusu
kufanyiwa vipimo vya magonjwa haya. Pia kujadili dalili wazipatazo
ambazo zinahusiana na magonjwa haya ya zinaa au endapo walijihusisha na
vitendo vya ngono isiyo salama. Hii ni muhimu kwa kuwa ni nadra kwa
magonjwa haya kufanyiwa uchunguzi, bali uchunguzi hufanyika wakati
mgonjwa anapoonyesha dalili na kusubiri dalili ugonjwa hugundulika
wakati umekuwa sugu.
Magonjwa ya zinaa hutibika, wajawazito walioambukizwa magonjwa kama
chlamydia, kisonono,kaswende na trichomoniasis hutibiwa kwa kutumia dawa
za kuandikiwa na daktari za antibiotiki ambazo ni salama kwa
wajawazito. Magonjwa yasababishwayo na virusi hutibiwa kwa dawa za
virusi (antviral medications), na juhudi mahususi uchukuliwa
kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, kwa kutumia dawa
maalum apewazo mama wakati wa ujauzito.
kwa maelezo na usahauri zaidi unaweza kunipigia simu kwa namba 0759324414, au unaweza kutufikia moja kwa moja katika vituo vyetu vilivyopo mikoani kwa ajili ya kupata ushauri na huduma ya matibabu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni