Jumamosi, 5 Novemba 2016

Nini Chanzo, Tiba & Kinga ya Maambukizi Sugu ya Njia ya Mkojo (Chronic UTI)?

urinary-tract-infection
MAAMBUKIZI sugu ya njia ya mkojo (chronic urinary tract infections – UTIs) ni maambukizi kwenye njia ya mkojo ambayo hayatibiki kwa urahisi au yanajirudia mara kwa mara.
 
Maambukizi haya yanaweza kuendelea kuathiri njia ya mkojo hata baada ya kupata matibabu sahihi au yanaweza kujirudia muda mfupi baada ya matibabu. 
Njia ya mkojo huunda mfumo wa mkojo ukiwa na ogani mbalimbali kama figo, ureta (mirija inayobeba mkojo kutoka kwenye figo kwenda kwenye kibofu cha mkojo), kibofu cha mkojo na urethra (mirija inayobeba mkojo kutoka kwenye kibofu cha mkojo kutoa nje). 

Maambukizi kwenye njia ya mkojo yanaweza kutokea sehemu yoyote ya mfumo wa mkojo. Ikiwa maambukizi yataathiri kibofu cha mkojo peke yake ni rahisi hali hii kutibika, isipokuwa maambukizi yakisambaa mpaka kwenye figo, unaweza kuumwa zaidi na pengine kulazwa hospitali. 


Ingawa maambukizi ya njia ya mkojo yanaweza kumpata yeyote, wakati wowote bila kujali jinsia na umri, maambukizi haya hutokea sana kwa jinsia ya kike. Tafiti ya National Institute of Diabetes and Digestive and Kidney Diseases (NIDDK) inakadiria kila wanawake watano kuna mmoja anasumbuliwa na maambukizi ya njia ya mkojo yanayojirudia mara kwa mara.
 
Nini Huongeza Hatari ya Maambukizi Sugu ya Njia ya Mkojo?
Maumbile: Maambukizi sugu ya njia ya mkojo huwapata sana jinsia ya kike kutokana na maumbile yao.

Kwanza, urethra ipo karibu sana na puru (rectum) kwa wanawake kitu kinachorahisisha bacteria kutoka kwenye puru kuingia kwenye urethra hasa ukichamba/kutawadha kwa kurudisha mkono kutoka nyuma kwenda mbele. Hii ni moja ya sababu kubwa ya watoto wadogo wa kike kupata maambukizi ya njia ya mkojo kwa kuwa bado hawajajifunza jinsi ya kuchamba vizuri.

Pili, urethra ya mwanamke ni fupi zaidi ikilinganishwa na ya mwanaume. Hii ina maana bacteria wana umbali mfupi zaidi wa kusafiri kufika kwenye kibofu cha mkojo ambapo wanaweza kuzaliana na kuongezeka kiurahisi na kusababisha maambukizi.
 
Aina ya Maisha: Kuna aina ya maisha ambayo yanaweza kukufanya uwe kwenye hatari zaidi ya kupata maambukizi sugu ya njia ya mkojo kwa urahisi. Kwa mfano kutumia diaphragm (mpira laini maalum unaowekwa ukeni wenye kizibo cha kuzuia mbegu za mwanamume kupenya ili kukutana na yai la mwanamke) inaweza kusukuma juu urethra na kufanya iwe vigumu kutoa mkojo wote baada ya kukojoa. Mkojo unaobaki kwenye kibofu huongeza uwezekano wa bacteria kuzaliana na kusababisha maambukizi.

Mfano mwingine ni pale mwanamke anapobadili muundo wa kinga ndani ya uke wake kwa kutumia vitu vyenye kemikali kuosha uke wake, zinazoua bacteria walinzi wa kwenye uke, kama sabuni, marashi au viua shahawa (spermicides). Pia, kunywa dawa za kuua bacteria mwilini huweza kuua bacteria walinzi kwenye uke. Hii inaweza kuongeza hatari ya kupata maambukizi sugu ya njia ya mkojo.
 
Kukoma hedhi: Kukoma hedhi husababisha mabadiliko ya homoni, ambayo mwisho husababisha kubadilika kwa hali ya bacteria walinzi ndani ya uke hivyo kufanya wafe kwa wingi na uke kukosa ulinzi na kufanya iwe rahisi kupata maambukizi ya njia ya mkojo mara kwa mara.
 
Aina za Maambukizi Sugu ya Njia ya Mkojo ni zipi?
Maambukizi ya njia ya mkojo husababishwa na bacteria. Mara nyingi bacteria huingia mfumo wa mkojo kupitia urethra na kisha huzaliana na kuongezeka zaidi kwenye kibofu cha mkojo. Ili kuelewa zaidi maambukizi haya jinsi yanavyotokea ni vizuri kugawanya maambukizi katika kibofu cha mkojo na maambukizi katika urethra.

Maambukizi katika kibofu cha mkojo (Cystitis) mara nyingi husababishwa na bacteria waitwao Escherichia coli. E.coli ni aina ya bacteria wanaoishi kwenye utumbo wa watu na wanyama wenye afya nzuri. Bakteria hawa wakiwa mahala pao hawana madhara, isipokuwa wakipata upenyo wa kutoka huenda njia ya mkojo na kusababisha maambukizi.

Mara nyingi hutokea pale mabaki ya kinyesi yasiyoonekana yanapoingia njia ya mkojo. Hii inaweza kutokea wakati wa kufanya ngono mfano mwanaume anapoingiza uume mbele na nyuma (njia ya haja kubwa). Kushiriki ngono ya matakoni kunaongeza hatari ya kupata maambukizi katika njia ya mkojo. Maambukizi pia yanaweza kutokea wakati wa kujitawadha unapopeleka mabaki ya kinyesi mbele.

Maambukizi katika urethra (Urethritis) yanaweza kusababishwa na bacteria kama E.coli, lakini pia yanaweza kusababishwa na magonjwa/maambikizi ya njia ya ngono (STI) kama pangusa, kisonono au klamidia. Hata hivyo, magonjwa/maambukizi ya njia ya ngono husababisha mara chache sana maambukizi ya njia ya mkojo.
 
Dalili za Maambukizi Sugu ya Njia ya Mkojo ni zipi?
Kukojoa mara kwa mara, mkojo uliochanganyika na damu au mkojo mzito sana, kuhisi mkojo kuchoma au maumivu wakati wa kukojoa, maumivu kwenye figo yaani chini ya mgongo au chini ya mbavu, maumivu chini ya kitovu au kwenye kibofu cha mkojo.
Ikiwa maambukizi yatasambaa hadi kwenye figo, yanaweza kusababisha kichefuchefu, kutapika, baridi, homa kali (zaidi ya nyuzi za Fahrenheit 101 au nyuzi za Centigrade 38.3), uchovu na kuchanganyikiwa.
 
Hali ikiwa Mbaya Kiasi Gani Ndio Nimuone Daktari?
Dalili za maambukizi ya njia ya mkojo zinaweza zisiwe kali mwanzoni, isipokuwa baadaye zikawa kali na kukufanya ujisikie vibaya. Ikiwa dalili zitakuwepo kwa zaidi ya siku 5 ni vyema ukamuona daktari. Pia, muone daktari haraka ikiwa mwili utachemka sana, ikiwa una mimba au kisukari.

Nini Madhara ya Muda Mrefu ya Maambukizi Sugu ya Njia ya Mkojo? Maambukizi sugu ya njia ya mkojo yanaweza kusababisha maambukizi kwenye figo, ugonjwa wa figo, kuharibika kwa figo hasa kwa watoto wadogo, kusambaa kwa bakteria kwenye damu (septicaemia) na kuongezeka hatari ya kuzaa watoto njiti kwa wajawazito.
Ninawezaje Kujikinga na Maambukizi Sugu ya Njia ya Mkojo?
Kojoa mara nyingi uwezavyo muda wowote unapojihisi kukojoa. Wakati wa kuchamba, safisha kwa kupeleka nyuma uchafu. Kunywa maji mengi kusafisha bakteria kwenye njia ya mkojo kila mara unapokojoa, vaa chupi iliyoundwa kwa pamba, epuka kuvaa nguo za ndani zinazobana sana. Epuka kutumi diaphragm kama njia ya uzazi wa mpango. 

KWA MATIBABU NA USHAURI ZAIDI UNAWEZA KUTUFIKIA LUPIMO SANITARIUM CLNIC AU UNAWEZA KUNIPIGIA SIMU SASA HIVI KWA NAMBA 0759324414 KARIBU SANA.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni